Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu
Kijaji akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 9 la mwaka la wataalamu
wa ununuzi na ugavi leo jijini Dodoma.
|
Na
Jonas Kamaleki- MAELEZO, Dodoma
Wataalamu wa Ununuzi
na Ugavi wametakiwa kujiepusha na vitendo vya rushwa na kuwa wazalendo,
wabunifu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Rai hiyo imetolewa
leo na Jijini Dodoma na Naibu Wairi wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji
wakati akifungua Kongamano la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi.
Amesema matokeo ya
ukaguzi yanaonyesha kuwa kuna viashiria vya rushwa kwenye miradi ya umma, kitu
ambacho kinatisha kwa maendeleo ya Taifa na hivyo kuwataka wataalaamu wa
manunuzi na ugavi kuepuka vitendo hivyo viovu.
Dkt. Kijaji amesema
kuwa program na miradi mingi ya Serikali haiwezi kufanyika bila kuhusisha
ununuzi na ugavi na hivyo kuwataka wataalamu hao kuwa waadilifu na kufanya kazi
kwa ujuzi na weledi.
“Mafanikio yetu
katika kuufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 yatatokana na umakini wetu, ubunifu
wetu na uzalendo kwa Taifa letu,” alisema Dkt. Kijaji.
Aliongeza kuwa
ubunifu ndio nguzo kuu ya mafanikio ya Taifa na kuongeza kuwa uzalendo wa hali
ya juu utumike katika kusimamia mipango na miradi ya Serikali.
Aidha, Dkt. Kijaji
amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais, Dkt. John
Pombe Magufuli imejipambanua katika kuwaletea wananchi maendeleo, hivyo
wataalamu wa ununuzi na ugavi hawana budi kutumia ujuzi wao kuhakikisha thamani
ya fedha katika miradi yote inakuwa halisi.
Akisisitiza kuhusu
ujenzi wa Tanzania ya viwanda, Dkt. Kijaji amesema kuwa viwanda vitachochea
utoaji wa ajira, ongezeko la pato la Taifa na pato la mtu mmoja mmoja, hivyo
kufanya maisha ya Watanzania kuwa bora.
“Viwanda vitaongeza
uzalishaji na kufanya nchi yetu kuuza bidhaa nyingi nje ya nchi na kuongeza
fedha za kigeni, na kwa mara ya kwanza tangu tupate uhuru Tanzania imekuwa na
fedha ya kigeni ya kutosha kuagiza bidhaa toka nje kwa kipindi kisichopungua
miezi sita na kuwa ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki,” aliongeza Dkt.
Kijaji.
Naibu Waziri Kijaji
amesititiza suala ubunifu kutiliwa mkazo ikizingatiwa kuwa Tanzania kwa suala
la ubunifu ipo chini ya ailimia 50, hivyo kuitaka Bodi ya Ununuzi na Ugavi
kuwekeza zaidi katika ubunifu ili kufikia maendeleo endelevu.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi, Sister, Dkt. Hellen
Bandiho, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha miaka mitatu
imekuwa na mafanikio makubwa katika utoaji elimu bure, kuboresha utoaji wa
huduma za jamii kama vile afya na uwajibikaji kwa watumishi umma, kuboresha
miundombinu na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ikiwemo ununuzi wa ndege
unaoendana na ufufuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).
Ameongeza kuwa hadi
kufikia Desemba Mosi 2018, Bodi imesajili jumla ya wataalamu 10,863 katika
ngazi mbalimbali za ununuzi na ugavi.
“Bodi ya Wataalamu wa
Ununuzi na Ugavi inatekeleza agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli la kuhamia Dodoma na tumefanikiwa kupata
ofisi za kupanga kwenye jingo la PSSSF, hivyo Bodi inatarajia kuhamia Dodoma
hivi karibuni baada ya utaratibu wa kiutawala kukamilika,”alisema Dkt. Bandiho.
Hili ni Kongamano tisa na linafanyika kwa siku tatu Jijini
Dodoma ambapo linahudhuriwa na washiriki kutoka mikoa yote ya Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni