Jumatatu, 29 Februari 2016

Jalada la maelezo fafanuzi: Lishe ya Mtoto nchini Tanzania



Jalada la maelezo fafanuzi: Lishe ya Mtoto nchini Tanzania

Hali ya lishe ya watoto
·   Tatizo la  utapiamlo hususani udumavu (kuwa na kimo kidogo ukilinganisha na umri) miongoni mwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 5, limepungua toka asilimia 50 mwaka 1992 hadi kufikia asilimia 35 mwaka 2014, ambapo imeathiri  watoto takriban milioni 2.7. Kulingana na vigezo viliyoainishwa na Shirika la Afya Duniani (mwaka 1995), tatizo la udumavu limepungua toka “hali ya juu kabisa” kufikia “hali ya juu”.
·   Hatua madhubuti kabisa za kuwakinga watoto dhidi ya udumavu zinafanyika katika kipindi cha dhana iliyoitwa ‘ dirisha la fursa ’ yaani kuanzia kutungwa kwa mimba, kipindi cha ukuaji wa mimba hadi mwisho wa kipindi cha miaka miwili ya uhai wa mtoto.
·   Tatizo la  utapiamlo mkali wa jumla au hali ya ukondefu kwa watoto ( kuwa na uzito mdogo ukilinganishwa na kimo cha mtoto) chini ya umri wa miaka 5 ilipungua toka asilimia 8 ngazi ya kitaifa mwaka 1992 hadi kufikia asilimia 4 mwaka 2014. Tatizo la utapiamlo mkali liko katika kiwango cha  “chini kabisa” kulingana na vigezo  vya  Shirika la Afya Duniani. Hata hivyo, visiwani Zanzibar, kiwango cha  utapiamlo mkali wa jumla kilbaki kuwa juu, na kinafikia asilimia 7.
·   Kulingana na idadi halisi, zaidi ya watoto 430,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano wanasumbuliwa na utapiamlo mkali wa jumla, miongoni mwao zaidi ya watoto  100,000 wana utapiamlo mkali sana, na kati ya asilimia 5-20 ya watoto hao wako katika hali hatarishi inayoongeza uwezekano wa kufa .
·   Tatizo la  upungufu wa uzito usiokuwa wa kawaida kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano limepungua toka asilimia 25 mwaka 1992 hadi kufikia asilimia 13 mwaka 2014, idadi ambayo inakaribia asilimia 12.5 ikiwa lengo ambalo serikali ya Tanzania imejiwekea.
·   Utapiamlo umetawanyika kwa viwango tofauti baina ya mikoa na jinsia tofauti nchini Tanzania, hasa ukiwaathiri zaidi wavulana, watoto wanaoishi katika jamii zenye mapato duni na miongoni mwa watoto wanaoishi katika mikoa mahsusi[1].
·   Mifano miwili ya taratibu muhimu za malezi ya watoto kwa ajili ya lishe bora katika maisha ya mtoto mchanga ni Unyonyeshaji na ulishaji wa chakula cha nyongeza , ila tabia na taratibu za ulishaji wa watoto wachanga na watoto wenye umri mdogo bado ni hafifu:
o  Kiwango cha unyonyeshaji mtoto maziwa ya mama pekee katika miezi 6 ya mwanzo  (EBF) miongoni mwa watoto wenye umri kati ya miezi 0-5 kiliongezeka toka asilimia 29 mwaka 1996 hadi kufikia asilimia 41 mwaka 2005, ila idadi ya asilimia hii haikubadilika na kubaki asilimia 42 mwaka 2014. Visiwani Zanzibar, ni asilimia 20 tu ya watoto wenye umri wa chini ya miezi 6 wananyonyeshwa bila kuchanganya maziwa ya mama na vitu vingine. Asilimia 51 ya watoto Tanzania Bara na asilimia 62 Visiwani Zanzibar wananyonyeshwa katika kipindi cha saa ya kwanza baada ya kuzaliwa;
o Kuhusu ulishaji watoto vyakula vya nyongeza, asilimia 25 ya watoto wenye umri wa kati ya miezi 6-23 wanapata chakula cha mchanganyiko wa vyakula mbalimbali kwa Tanzania Bara dhidi ya asilimia 12 Visiwani Zanzibar. Hali kadhalika, ni asilimia 20 tu ya watoto Tanzania Bara wanapata milo yenye mchanganyiko wa vyakula mbalimbali na kulishwa idadi ya milo inayokubalika dhidi ya asilimia 8 Visiwani Zanzibar. Idadi ya watoto kitaifa wanaopata wastani wa milo inayopendekezwa kwa siku ni asilimia 66 kwa Tanzania bara na  na asilimia 54 Visiwani Zanzibar.  
·   Upungufu ya virutubishi ni tatizo la kawaida na mikakati ya kushughulikia tatizo hilo inaonyesha maendeleo yanayo badilika mara kwa mara:
o Tatizo la upungufu wa damu miongoni mwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ulipungua toka asilimia 72 mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 59 mwaka 2010;
o Theluthi moja ya watoto wanaathirika na upungufu wa vitamini (asilimia 33);
o Ni asilimia 8.3 tu ya wanawake walio katika  umri wa kuzaa wenye watoto chini ya miaka mitano waliwahi kutumia vidonge vya madini ya chuma na asidi ya foliki (iron-folic acid)  katika kipindi cha siku 90 au zaidi wakati wa ujauzito wao uliopita, kama inavyoagizwa na Shirika la Afya Duniani (WHO);
o Vitamini A ni muhimu sana kwa ajili ya uimarishaji wa mfumo wa kinga, na matumizi ya ziada ya Vitamini A yanaweza kupunguza vifo vya watoto kabisa. Uwiano wa watoto wenye umri kati ya miezi 6-59 wanaopata Vitamini A ya ziada ulipanda toka asilimia 61 mwaka 2010 na kufikia asilimia 72 mwaka 2014. Hata hivyo, matumizi yake yalipungua Zanzibar toka asilimia 79 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 61 mwaka 2014.
o Uwiano wa watoto wenye umri kati ya miezi 12-59 wanaopata vidonge vya kukabiliana na minyoo uliongezeka toka asilimia 50 mwaka 2010 hadi asimilia 71 mwaka 2014, ila ulipungua Visiwani Zanzibar toka asilimia 72 mwaka 2010 na kufikia asilimia 68 mwaka 2014[2].

Sababu na madhara ya  lishe duni
·   Watoto wanaweza kupatwa na utapiamlo ikiwa watasumbuliwa na magonjwa yanayosababishwa na lishe duni au ikiwa hawana uwezo wa kula chakula cha kutosha na cha mchanganyiko. Mara nyingi sababu hizi mbili zinatokea kwa pamoja na zinatokana na sababu nyingi zilizojificha, zikijumuisha upatikanaji usiojitosheleza au kutokupatikana kwa chakula au kutokuwepo na fursa za kiuchumi, huduma duni za kiafya, mazingira yasiyokuwa rafiki kiafya na shughuli za malezi zisizotosheleza  kwa watoto na wanawake.
·   Watoto wenye utapiamlo wana athirika zaidi na magonjwa ya maambukizi na viwango vya juu vya vifo miongoni mwa watoto hawa. Zaidi ya hayo, utapiamlo unaathiri ukuaji wa ubongo na huwa unapunguza uwezo wa kiakili na wa kujifunza miongoni mwa watoto, hali ambayo inasababisha uwezo hafifu mashuleni na kupunguza mapato ya kiuchumi wanapokua watu wazima.
·   Utapiamlo unatafsiriwa katika upotevu wa kiuchumi wa mtu mmoja mmoja hadi kufikia asilimia 10 ya Jumla ya Pato la Taifa (GNP) na kuathiri ukuaji wa uchumi wa nchi.
·   Tatizo la utapiamlo kwa watoto linaweza kupungua kwa kupitia mtazamo unaojumuisha sekta nyingi, ukiunganisha hatua maalumu za kupanua huduma za lishe zinazotoa manufaa ya moja kwa moja kwa jamii kisekta au huduma zinazohusiana na lishe zinazofanywa na sekta mbalilmbali pamoja na kuimarisha mazingira yatakayoleta ufanisi katika kuboresha lishe .


[1] Asilimia 58 ya watoto waliodumaa wako katika mikoa ya 10: Kagera, Kigoma, Mbeya, Mwanza, Dodoma, Morogoro, Geita, Dar-Es-Salaam, Tabora na Ruvuma. Wengi wa watoto wanaoathirika na utapiamlo mkali wanapatikana Dar es Salaam, Rukwa, Mwanza, Simiyu.
[2] Takwimu zote katika jalada hili la maelezo ni matokeo ya tafiti zInazohusu Ongezeko la Watu na taarifa za Kiafya, tafiti zinazofanyika kila baada ya miaka 5 nchini Tanzania toka Utafiti wa Kitaifa wa Lishe wa mwaka 2014

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa

Kumbukumbu la Blogu