Jumatatu, 29 Februari 2016

MFULULIZO WA MAKALA ZA “LANCET” KUHUSU UNYONYESHAJI MAZIWA YA MAMA



MFULULIZO WA MAKALA ZA “LANCET” KUHUSU UNYONYESHAJI MAZIWA YA MAMA

Ujumbe Maalum na Matokeo
·         Kunyonyesha maziwa ya mama kuna faida kubwa kwa wanawake na watoto kwenye nchi zenye vipato vya chini na vya juu, na ushahidi sasa ni imara zaidi kuliko siku za nyuma. 

·         Faida za kiafya na kiuchumi za kunyonyesha maziwa ya mama ni kubwa: kuongeza viwango vya unyonyeshaji maziwa ya mama kunaweza kuokoa maisha ya  maelfu ya watu na kuongeza  mabilioni ya dola kwenye uchumi wa dunia kila mwaka. 

·         Kuongeza viwango vya unyonyeshaji maziwa ya mama duniani kote ni kichochezi cha msingi cha kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Kunyonyesha maziwa ya mama kunachangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha lishe, elimu, na afya ya mama mjamzito na mtoto na kuendelea kuishi kwa mama na mtoto.

·         Maendeleo kwa kasi yanawezekana, na tunajua nini kinahitaji kufanyika—nchi nyingi zaidi zinahitaji kuwekeza kwenye sera na mipango ambayo inaunga mkono maamuzi ya wanawake kunyonyesha maziwa ya mama.

Kunyonyesha maziwa ya mama kuna faida nyingi sana kwa wanawake na watoto, bila kujali kama wanaishi kwenye nchi yenye kipato cha juu au cha chini au kwenye kaya tajiri au maskini.

·         Kunyonyesha maziwa ya mama kunaokoa maisha na kuboresha afya.
o Kama njia ya kuwapa watoto  lishe iliyotengenezwa kikamilifu, maziwa ya mama ni dawa bora zaidi inayotibu kwa kuangalia mahitaji binafsi ya lishe ya mtoto.
o Kuboresha unyonyeshaji kunaweza kuokoa takriban maisha 820,000 kwa mwaka,  87% kati yao wakiwa watoto wachanga wenye umri wa chini ya miezi 6.
o Karibu nusu ya matukio yote ya kuhara na theluthi moja ya maambukizo yote ya njia ya hewa yanaweza kuzuilika kwa kuongeza kiwango cha kunyonyesha maziwa ya mama kwenye nchi zenye kipato cha chini na cha kati. 
o Kuna ushahidi mkubwa zaidi kuwa kunyonyesha maziwa ya mama kunapunguza kuwepo  kwa matatizo ya unene/uzito mkubwa na kisukari baadaye maishani.

·         Kunyonyesha maziwa ya mama kunawaandaa watoto kuwa na maisha yenye  ustawi ukubwani. 

o Kunyonyesha maziwa ya mama kumehusishwa na kufanya vizuri zaidi kwenye vipimo vya upeo wa kiakili kwa watoto na vijana (wastani wa alama 3), kwa kuzingatia mchango wa mama katika upeo wa kiakili wa mtoto.
o Baadhi ya tafiti zinaonyesha kwamba kuwa na akili kama matokeo ya kunyonyeshwa maziwa ya mama kunapelekea kuwa na maendeleo mazuri ya kielimu, kipato na uzalishaji mkubwa katika kipindi cha muda mrefu.
o Kidunia, makadirio ya gharama ya upeo mdogo wa kiakili unaohusika na kutonyonyeshwa maziwa ya mama ni jumla ya takriban dola za kimarekani bilioni 300 kwa mwaka (ikiwakilisha 0.49% ya pato la jumla la nchi duniani, au GNI).
-        Nchi zenye kipato cha juu zinapoteza zaidi ya dola bilioni 230 kwa mwaka  (0.53% yapato la jumla la nchi) kwa sababu ya viwango vidogo vya unyonyeshaji maziwa ya mama.
-        Nchi zenye kipato cha chini na cha wastani zinapoteza zaidi ya dola bilioni 70 kwa mwaka (0.39% ya pato la jumla la nchi) kwa sababu ya viwango vidogo vya kunyonyesha maziwa ya mama.

·         Kunyonyesha maziwa ya mama pia kuna faida kwa afya ya mama.
o Kwa kila mwaka ambao mama ananyonyesha, uwezekano wa yeye kupata saratani ya matiti ya hatua ya pili unapungua kwa 6%. Kunyonyesha maziwa ya mama pia kunapunguza hatari ya kupata saratani ya mfuko wa mayai.
o Viwango vya sasa vya kunyonyesha maziwa ya mama tayari vinazuia vifo karibu 20,000 vinavyotokana na saratani ya matiti kila mwaka, na vifo vingine 20,000 vinaweza kuzuiliwa kwa kuboresha namna za kunyonyesha maziwa ya mama.

Pamoja na faida za kiuchumi,  na kiafya za kunyonyesha maziwa ya mama zinakadiriwa kuchangia  kushusha gharama za mwaka za huduma ya afya kwa jumla ya dola  milioni 312 nchini Marekani, dola milioni  48 nchini Uingereza, dola milioni  6 nchini Brazil na dola milioni 30.3 Uchina mjini.
Ingawa kuna ushahidi huu mkubwa zaidi, wanawake duniani kote hawana msaada wanaohitaji kunyonyesha maziwa ya mama.

·         Sheria zisizokidhi  au kukosekana kabisa kwa sheria zinazolinda au kutetea kipindi cha uzazi kunazuia wanawake wengi kunyonyesha maziwa ya mama kwa kiasi kinachotakiwa.

o Likizo fupi ya uzazi (mfano wiki6) kwa baadhi ya nchi inaongeza uwezekano wa kutonyonyesha maziwa ya mama  au kuacha kunyonyesha maziwa ya mama mapema kwa 400%.
o Ni asilimia 23% (chini ya robo) ya nchi zote duniani zinakidhi mapendekezo ya Shirika la Kimataifa la Kazi ya kuweka majuma 18 kwa ajili ya likizo ya uzazi.  

·         Mapungufu  kwenye ujuzi na uelewa wa watoa huduma ya afya mara nyingi huwaacha wanawake bila taarifa au msaada sahihi. 

·         Mila na desturi za kifamilia na kijamii pia zina ushawishi mkubwa kwenye maamuzi wa wanawake kunyonyesha maziwa ya mama. Yatupasa kujenga hali mpya itakayowawezesha  wanawake kuungwa mkono kuhusu maamuzi yao ya kunyonyesha maziwa ya mama – nyumbani, kazini na kwenye jamii. 

·         Uuzaji unaofanywa na tasnia kubwa na inayozidi kukua ya chakula cha mbadala ya maziwa ya mama pia unadhoofisha kunyonyesha maziwa ya mama.
o Kati ya mwaka 2014 na 2019, mauzo ya dunia ya chakula cha mbadala ya maziwa ya mama yanatarajiwa kuongezeka kutoka dola bilioni 45 hadi dola bilioni 71. 

o Mashariki ya Kati, Afrika, na kanda ya Asia ya Pasifiki ndio maeneo ambayo kukua kunategemea kuongezeka, ikikadiriwa kuongezeka kwa asilimia 7% na 11%.



Viwango vya kunyonyesha maziwa ya mama havijaongezeka kwa kiasi kikubwa katika miongo miwili iliyopita, na nchi nyingi hazielekei kufikia malengo yaliyowekwa kidunia. 

·         Watoto wote walio chini ya miezi 6 wanapaswa kunyonyeshwa maziwa ya mama bila kuchanganyiwa chakula kingine kwa miezi 6 ya mwanzo, lakini ni 37% tu wanatimiza lengo hili kwa sasa. Lengo la dunia ni kuongeza viwango vya kunyonyesha maziwa ya mama bila kuchanganyiwa chakula kingine kwa miezi 6 ya kwanza ifike angalau 50%.
·         Kiwango kidogo cha kunyonyesha maziwa ya mama kulingana na mapendekezo kunaathiri nchi zenye kipato cha juu na nchi zenye kipato cha chini pia.Unyonyeshaji maziwa ya mama ni mojawapo ya viashiria vichache vya kiafya ambapo nchi zenye kipato cha chini zinakaribia kufikia mapendekezo ya kimataifa kuliko nchi zenye kipato cha juu. 
o Kwa kila mara Pato la Jumla la Ndani linavyoongezeka mara mbili zaidi, unyonyeshaji maziwa ya mama kwa miezi 12 unapungua kwa alama za asilimia 10. 
o  Chini ya  20% ya watoto kwenye nchi zenye kipato cha juu wananyonyeshwa maziwa ya mama kwa miezi 12.
o Kwenye nchi zenye kipato cha chini na cha wastani, chini ya 40% ya watoto wachanga walio chini ya miezi 6 wananyonyeshwa maziwa ya mama bila kuchanganyiwa chakula kingine, na theluthi mbili za watoto kati ya miezi 6 na miaka 2 wanapata maziwa ya mama. 

Akina mama wana uwezekano wa mara 2.5 zaidi kunyonyesha maziwa ya mama pale ambapo unyonyeshaji maziwa ya mama unalindwa, unahamasishwa na unaungwa mkono.

·         Mipango ya kuunga mkono inajumuisha ushauri nasaha kwa mtu mmoja  mmoja au elimu ya vikundi, kutoa msaada wa jinsi ya kunyonyesha maziwa ya mama baada ya  kujifungua, na mafunzo kuhusu maziwa ya mama kwa ajili ya wafanyakazi wa afya. 
·         Viwango vya kunyonyesha maziwa ya mama vinaweza kuboreshwa kwa kiasi kikubwa kwa muda mfupi sana.Kifurushi chenyemiongozo ya kufundishia, sera na mipango ya kusaidia akimama kwenye vituo vya afya, majumbani, na hata makazini vinaonyeshwa kuwa na mchango mkubwa zaidi. Hivyo inatupasa:
o Kusambaza taarifa sahihikuhusu thamani ya kunyonyesha maziwa ya mama kama afua yenye nguvu kwa ajili ya afya na maendeleo, yenye manufaa kwa watoto na akinamama.
o Kujenga mitazamo mizuri katika jamii kuhusu kunyonyesha maziwa ya mama  na kusisitiza kuhusu kuwa na mtazamo chanya wa kunyonyesha maziwa ya mama.
o Kuonyesha nia ya kisiasaya kuunga mkono unyonyeshaji maziwa ya mama.
o Kudhibiti tasnia ya chakula mbadala wa maziwa ya mama kwa  kufuatilia na kutekeleza kisheria Kanuni ya Kimataifa ya Uuzaji wa Chakula Mbadala ya Maziwa ya Mama.
oKueneza na kufuatilia mikakati ya unyonyeshaji maziwa ya mama na mienendo katika kunyonyesha maziwa ya mama.
o  Kuimarisha hatua za kisera kuhakikisha sheria zinazowalinda  wanawake katika kipindi cha uzazi zinaboreshwa na afua za mahali pa kazi zinatekelezwa na kuwa huduma za afya na uzazi ni rafiki kwa kuwawezesha kinamama kunyonyesha maziwa ya mama na zinafuata Kanuni.



Kujitoa na kuwekeza katika afya wa wanawake na watoto – pamoja na kunyonyesha maziwa ya mama – kuwezesha kufanikisha lengo la dunia litakalopelekea kuwepo na maendeleo katika malengo mengine ya afya na maendeleo.

·         Kuwekeza kwenye kuinua ubora na utoaji huduma kwa maeneo mengi zaidi kwa wanawake na watoto wao wachanga kutapelekea kupata faida ya mara tatu zaidi ya mtaji, kwa kuzuia 54% ya vifo vya mama wajawazito, 71% ya vifo vya watoto wachanga na 33% ya watoto wanaofia tumboni.
·         Afya ya wanawake, watoto na vijana ni mzunguko ambao husababisha mabadiliko yanayohitajika ili kuunda hali ya afya ya baadaye yenye ustawi zaidi,imara zaidi na endelevu kwa ajili ya kila mmoja.
·         Kumekuwa na maendeleo makubwa katika miaka 15 iliyopita hususani  kwenye afya ya uzazi, mama mjamzito, watoto wachanga, na vijana  (RMNCAH), ambayo ni muhimu katika kuendeleza Mkakati wa Dunia wa Kuimarisha Afya ya Wanawake, Watoto na Vijana na malengo yake ya Kuendelea Kuishi, Kustawi, na Kubadilika yakijumuisha harakati ya Kila Mwanamke Kila Mtoto. Kuendelea kuishi, afya na ustawi wa wanawake, watoto na vijana ni muhimu katika kutokomeza umaskini uliokithiri, kukuza maendeleo nauthabitina kutimiza Malengo mapya ya Maendeleo Endelevu.

Mwaka huu The Lancet imeandaa mkusanyiko wa ushahidi mpya ambao utakazia kwenye mada muhimu zilizotajwa na Mkakati wa Dunia wa Kuimarisha Afya ya Wanawake, Watoto na Vijana. Hii ni pamoja na kuzindua Mfululizo wa makala  kuhusu Watoto Wanaofia Tumboni (imeshatolewa mwezi Januari 2016), Kunyonyesha Maziwa wa Mama (Januari 2016), ripoti kuhusu Tume ya Afya na Ustawi wa Vijana iliyoandaliwa na The Lancet(itatolewa mwezi Mei,2016), na baadaye kutakuwa na  Mfululizo kuhusu Afya ya Mama Mjamzito, Maendeleo na Makuzi ya Awali ya Mtoto, Afya ya Wanawake na Mama na Mtoto Kuendelea Kuishi. Makala ya Kila Mwanamke Kila Mtoto itajulisha nchi na wabia kuhusu ushahidi huu katika kusaidia utekelezaji wa Mkakati wa Dunia

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Jumla ya Mara Iliyotazamwa

Kumbukumbu la Blogu