Hayo yamebainishwa na Meneja Mwandamizi wa Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Kanda ya Magharibi-Tabora, Bw. Emmanuel Adina
katika Maonyesho ya Wiki ya Vijana yanayofanyika Kitaifa mjini Tabora.
Adina ameongeza kuwa viongozi wa dini zote wamekuwa
mstari wa mbele katika kuhamasisha waumini wao kujiunga na CHF ili kuwa
nauhakika wa kupata huduma stahiki ya matibabu.
Aidha amesema kuwa viongozi hao wamekuwa
wakihamasisha watu wao misikitini, kwa upande wa Waislam na makanisani kwa
Wakristo. Hadi sasa jumla ya kaya 38,000 wamejiunga na Mfuko huo huku lengo likiwa
ni kufikia asilimia 30 ya waliojiunga na
CHF ifikapo Juni 2015
Meneja huyo ameitaja wilaya ya Igunga kuongoza
katika uhamasishaji wa wananchi kujiunga na CHF. “Namshukuru sanaMkuu wa Wilaya
ya Igunga, Bw. Elibariki Kingu kwa mchango mkubwa anaoutoa kwa wana Igunga
kujinga na Mfuko huo ambapo jumla ya kaya 9,000 wilayani Igunga zimejiunga na
CHF ambayo ni idadi kubwa kutokana na uhamasishaji wa Mkuu wa wilaya”. Alisema
Bw. Adina.
Ameongeza kuwa Bw. Adina amezitaja wilaya nyingine
ambazo kaya nyingi zimejiunga na Mfuko huo kuwa ni Nzega, Uyui,Urambo na
Sikonge. Katika wilaya hizo kinachosaidia zaidi watu kujiunga ni kuwepo
wilayani humo vyama vya ushirika vya msingi vya tumbaku.
Zipo pia changamoto NHIF inayokutana nazo kuhusiana
na wana Tabora kujiunga na CHF. Changamoto hizo Meneja huyo amezitaja kuwa ni
kipato kidogo cha wakazi wa Tabora inayotokana kuwa baadhi ya wilaya hazina zao
kuu la biashara la kuwapatia kipato cha uhakika, kutokuwepo na elimu ya kutosha
ya mifumo ya Bima na pia ukosefu wa dawa na vifaa tiba katika mahospitali,
zahanati na vituo vya afya.
Kwa upande mwingine, Afisa Masoko na Elimu kwa Umma
wa NHIF, Bi Catherine Kameka amewataka wananchi wajiunge kwa wingi na Mfuko wa
Afya wa Jamii na Bima ya Afya ili waepuke usumbufu wa kukosa matibabu wakati
wanapokuwa wanahitaji matibabu na hawana pesa. Amesema ugonjwa hauna msimu,
unaweza kujitokeza wakati wowote hivyo ukiwa kwenye mifumo ya Bima ni rahisi
kuhudumiwa.
Ameongeza kuwa huduma zinazotolewa kwa wanachama wa NHIF
zimeboreshwa na kuvutia wanachama wengi zaidi ikilinganishwa na ilivyokuwa
wakati mfuko unaanzishwa. Hivyo amewataka wanaTabora wachangamkie fursa hiyo
ili wawe na afya njema wakati wote kwa maana mtu akiwa na afya safi anaweza
kujishughulisha kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni