Mkuu
wa mkoa wa Arusha, Mhe Mrisho Gambo amewaagiza Wakuu wa Wilaya tatu za Mkoa wa
Arusha zinazotekeleza mradi wa mabadiliko
ya hali ya hewa na tabia ya nchi kuwa Wenyeviti wa kamati za mradi huo ili
kuharakisha utekelezaji wake katika
maeneo hayo.
Akizungumza
katika kikao cha kutambulisha mradi huo wa awamu ya Pili utakaofanya kazi
katika wilaya za Ngorongoro, Monduli na Longido za Mkoa wa Arusha kwa kipindi
cha miaka mitano kuanzia mwaka 2016 hadi 2021 alisema kuna haja ya kuimarisha
usimamizi wa mradi huu ili kuwajengea uwezo
wanajamii katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia
nchi ili mradi huu uweze kuleta Tija iliyokusudiwa.
Alisema
awali kamati hizo zilikuwa zikisimamiwa na Maafisa Mipango katika halmashauri
hizo ila kutokana na majukumu yao ameonyesha wasiwasi iwapo wanaweza kuusimamia
ipasavyo hivyo aliwataka Wakuu wa wilaya
kuwa vinara wa kuusimamia na kuratibu kwa karibu ili kuleta mapinduzi katika maeneo ya wafugaji na
kuhakikisha wanatengeneza mfumo imara na utekelezaji wa mradi huo unafanikiwa kuanzia
ngazi ya kijiji.
“Nahitaji
kuona halmashauri ambazo zinatekeleza mradi huu ifikapo mwezi Novemba ziwe
zimeshaanza kutekeleza majukumu yake bila vikwazo vyovyote na nipate taarifa
zake mara kwa mara ili fedha zilizotolewa na wafadhili zilete matokeo
chanya,”alisema Gambo
Akizungumza wakati wa Kikao hicho Mwakilishi Mshauri wa Taasisi ya
Kimataifa ya Mazingira na Maendeleo (IIED) Alais Morindat alisema kuwa mabadiliko ya hali ya hewa imekua ni
tishio kubwa kwa wananchi haswa wa maeneo haya ya wafugaji na ndio maana
tulianza na Halmashauri hizi kutokana na athari zilizojitokeza katika jamii za wafugaji
ambapo mifugo mingi katika maeneo yao ilipoteza uhai.
Aliongeza kuwa mradi huu unatofauti na miradi
mingine tuliyoizoea kwa sababu Jamii inakuwa na nafasi ya kuamua jinsi Fedha za
Mradi zitakavyotumika huku malengo ya mradi yakiwa ni kuijengea uwezo Ofisi ya Raisi –TAMISEMI
katika maeneo makubwa mawili ambayo ni uimarishaji wa taasisi katika
uratibu wa mradi na uwezo wa kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kuziwezesha
mamlaka za serikali za mitaa hapa nchini ziweze kutoa elimu kwa jamii
kutambua na kutekeleza Miradi ya kukabiliana na athari ya mabadiliko ya
hali ya hewa na tabianchi.
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo hususan Shirika la
Kimataifa la Mazingira na Maendeleo (IIED), Haki Kazi Catalyst (HKC), Jumuiko
la Maliasili Tanzania(TNRF) chini ya ufadhili wa Serikali ya Uingereza (UK-aid)
na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo (UNCDF LoCAL) itatekeleza mradi huu
katika Halmashauri 15 huku zaidi ya Bilioni 6 zinatarajia kutumika katika mradi
huu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni