MAJALIWA:
SERIKALI KUSAKA WALIOKULA FEDHA ZA WATUMISHI HEWA
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeamua kupambana na wala rushwa ili
kiasi kidogo cha rasilmali kilicholengwa kiweze kuwafikia wananchi.
Ametoa
kauli hiyo jana (Jumamosi, Mei 14, 2016) wakati akizungumza na Watanzania
waishio Uingereza kwenye mkutano uliofanyika kwenye Ubalozi wa Tanzania jijini
London, Uingereza.
“Jambo
tuliloamua kuanza nalo ni kupambana na rushwa. Tumeamua kufanya hivyo ili
kurudisha umoja na maelewano miongoni mwa Watanzania, tunataka tuibadili
Tanzania ili iwe ni ya Watanzania wote… tumechoka kuambiwa sehemu fulani mradi
umekamilika halafu ukienda kuangalia hukuti kitu na fedha ile haipo,” alisema
huku akishangiliwa.
Akizungumzia
zoezi la kusaka watumishi hewa, Waziri Mkuu alisema Serikali itawashughulikia
wale wote waliohusika na zoezi hilo. “Wafanyakazi hewa wamefikia zaidi ya
10,000 na tumeokoa zaidi ya sh. bilioni 4.5 zilizokuwa zikipotea kila mwezi.
Tukikamilisha zoezi la kusaka watumishi hewa, sasa tutataka kujua ni akina nani
walikuwa wakipokea fedha hizo. Waliohusika tutashughulika nao,” alisisitiza.
Alisema
hivi sasa Serikali inalenga kuwa na watumishi ambao wanafanya kazi kwa
uaminifu, uadilifu na uwajibikaji mahali pa kazi. “Hiki ndicho kipaumbele cha
Serikali ya awamu ya tano na tena zoezi hili litakuwa endelevu”, alisema Waziri
Mkuu.
Akizungumzia
kuhusu ukuaji wa uchumi, Waziri Mkuu ambaye alikuwa London kuhudhuria mkutano
uliojadili mapambano dhidi ya rushwa kwa niaba ya Rais Dk. John Pombe Magufuli,
alisema lengo la Serikali hivi sasa ni kuona kuna ukuaji wa uchumi unaoenda
sambamba na huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Alisema
viwanda vingi viliuzwa na watu waliovinunua wakageuza kuwa ni maghala ya
kufugia wanyama. Sisi tunataka vifufuliwe ili teknolojia mpya na za kisasa zije
Tanzania. Nafasi ya kuwekeza iko kwa Watanzania wote walioko nyumbani na ninyi
mlioko nje,” alisema.
Alisema
ardhi ipo ya kutosha na akawataka wawaalike marafiki zao waje kuwekeza nchini,
ili mradi wawe ni watu makini, wenye nia ya dhati ya kuwekeza nchini na wenye
mitaji na siyo madalali (middlemen). “Tunataka usindikaji wa mazao na bidhaa
ufanyike nchini mwetu badala ya kupeleka mazao ghafi nje ya nchi, kwa njia hiyo
tutakuwa pia tumezalisha ajira kwa watu wetu,” alisema.
“Kuna
Watanzania wanaishi Botswana, Ujerumani na Poland wameshaleta wawekezaji
nchini. Kwa mfano wa Poland wameleta mradi wa umeme katika vijiji vitani
wilayani Ileje. Kwa hiyo ninyi endeleeni kuishi Uingereza lakini mhakikishe
kuwa ukaaji wenu hapa, unaleta tija kule nyumbani. Kumbukeni Tanzania na muwe
tayari kuihudumia Tanzania,” alisema.
“Serikali
inaamini itanufaika na uwepo wenu hapa Uingereza. Muweke kipaumbele cha
kuwekeza nyumbani na mkishindwa mtutafutie marafiki zenu. Mwenye uwezo andaa
andiko la mradi halafu uwasiliane na Balozi ili akusaidie kutafuta wahusika
kule nyumbani,” aliwaasa.
Akijibu
swali kuwa ana maoni gani juu ya Bunge kutorushwa ‘LIVE’, Waziri Mkuu alisema
hatua hiyo ilichukuliwa ili kuwawezesha watu kufanya kazi kama ambavyo
kaulimbiu ya Mhe. Rais Magufuli ya Hapa Kazi Tu inavyosema.
“Bunge
la Tanzania lilikuwa ni bunge pekee katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na
duniani ambalo lilikuwa likirushwa LIVE kuanzia asubuhi hadi usiku. Ina maana
katika kipindi cha Bunge la bajeti, ambalo linaendeshwa kila siku kwa miezi
mitatu, Watanzania nao wangekuwa LIVE kwa miezi mitatu,” alisema.
“Tulilazimika
kujifunza kutoka kwenye mabunge mengine. Hivi hapa Uingereza mnaangalia Bunge
live kila siku?” alihoji Waziri Mkuu na kujibiwa kuwa linarushwa LIVE kwa
pipindi kisichozidi dakika 15 wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu tu.
Akitoa
ufafanuzi, aliwaeleza kwamba Bunge la Tanzania linarusha ‘LIVE’ kila siku
asubuhi wakati wa maswali ya kawaida na Alhamisi asubuhi wakati wa maswali kwa
Waziri Mkuu lakini mijadala yote hurekodiwa na kuhaririwa na kisha kurushwa
kuanzia saa 8-9 mchana na saa 3-4 usiku kwa siku husika.
Kwa
Watanzania wanaopenda kufanya kazi na wanapenda kufuatilia mambo ya Bungeni,
walikuwa hawaoni LIVE coverage jwa sababu walikuwa kazini lakini sasa hivi
wanaweza kufuatilia masuala ya bunge kwani muda wa jioni uliopangwa mtu anakuwa
ametoka kazini na anaweza kuangalia televisheni akiwa nyumbani baada ya kutoka
kazini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, MEI 15, 2016.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni