HOTUBA
YA MHE. KASSIM MAJALIWA MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI
WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA PILI WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA TAREHE 5 FEBRUARI, 2016
I: UTANGULIZI
(a)
Masuala ya Jumla
Mheshimiwa
Spika,
1.
Kwanza
nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutujalia afya njema na uwezo katika kutenda
yote yaliyo mema. Tumekuwepo hapa kwa
takriban siku 11 katika shughuli za Mkutano wa Pili wa Bunge lako Tukufu. Ni
jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha
salama siku ya leo.
2.
Tumekutana
hapa tukiwa tumeshuhudia uundwaji wa Serikali unaoendelea ambapo Mheshimiwa Dkt
John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya uteuzi wa
Baraza jipya la Mawaziri ambao ni Waheshimiwa
Wabunge wenzetu. Niruhusu nitumie nafasi hii ya awali kuwapongeza Mawaziri na
Naibu Mawaziri wote ambao wameteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali
ya Awamu ya Tano.
(b)
Chaguzi
Mbalimbali
Mheshimiwa
Spika,
3.
Katika
Mkutano huu, tumeweza kufanya Chaguzi za Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa
Kamati za Kudumu za Bunge. Vilevile, tumefanya
chaguzi za Wenyeviti wa Bunge letu na Wajumbe wa kutuwakilisha katika Taasisi
mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa. Kwa
vile orodha ni ndefu, napenda nitumie nafasi hii kuwapongeza kwa dhati kabisa
na kwa ujumla wao wote waliogombea nafasi hizo na kushinda. Ni matarajio yangu kwamba tutatumia nafasi
hizo vizuri katika kuleta ushirikiano, mshikamano na kufanya kazi pamoja kama
Wawakilishi wa Wananchi na kutekeleza majukumu yetu kama Wabunge ndani ya Bunge
hili.
(c)
Maafa na Ajali
Mheshimiwa Spika,
4.
Tarehe
27 Januari, 2016 wakati Bunge lako Tukufu likiendelea na Vikao, Waheshimiwa
Wabunge walipewa taarifa ya kusikitisha ya kuzama kwa Kivuko cha Kilombero, ambapo
katika tukio hilo watu walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa. Aidha, mali za
abiria zimepotea. Wakati huo huo, mvua zinazoendelea kunyesha nchini katika
baadhi ya maeneo zimesababisha mafuriko, vifo, uharibifu wa mali ikiwemo mazao
na miundombinu. Katika baadhi ya maeneo, mvua hizi zimesababisha njaa na athari
nyingine kwa jamii.
5.
Pamoja
na maafa ya mvua na mafuriko, wapo wananchi waliofariki na wengine kupata
ulemavu katika ajali mbalimbali za vyombo vya usafiri. Nitumie fursa hii kuwapa
pole wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika matukio yote hayo. Aidha,
napenda kuwatakia afya njema wote waliopata majeraha. Kwa wale wote waliopoteza
maisha tunawaombea Roho zao zilale mahali pema peponi - Amina.
6.
Kuhusu
uharibifu wa miundombinu, tunazo taarifa za uharibifu mkubwa wa Miundombinu katika
maeneo kadhaa. Napenda kulihakikishia
Bunge lako Tukufu kwamba Serikali itafanya kila liwezekanalo kurekebisha miundo
mbinu ya barabara iliyoharibika. Tunatambua gharama kubwa inayohitajika, lakini
ni wajibu wetu kama Serikali kuhakikisha Wananchi wanapata huduma muhimu hasa za
mawasiliano kati ya eneo moja na jingine.
(d)
Maswali
Mheshimiwa
Spika,
7.
Leo
tunahitimisha Mkutano wetu wa Pili wa Bunge tukiwa tumefanya shughuli
mbalimbali ndani ya Bunge letu. Katika
Mkutano wetu, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kuuliza maswali ya kawaida
na yale ya papo papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Jumla ya maswali 115 ya msingi na 307 ya nyongeza
yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali.
(e)
Mjadala wa Hotuba ya
Rais
Mheshimiwa
Spika,
8.
Katika
Mkutano huu moja ya agenda iliyochukua nafasi kubwa ni Hoja ya Serikali ya
kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Maufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Hoja hiyo
tuliihitimisha vizuri na kwa mafanikio makubwa.
Kazi kubwa iliyoko mbele yetu ni kutekeleza yale tuliyokusudia kama
wajibu wetu. Napenda kuwapongeza tena
Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushiriki katika mjadala wa Hotuba hiyo vizuri. Nichukue tena nafasi hii kuliahidi Bunge lako
Tukufu kwamba michango ya Waheshimiwa Wabunge na maoni yao yatazingatiwa kwa
utekelezaji.
II: MPANGO WA TAIFA WA MAENDELEO
Mheshimiwa Spika,
9.
Katika
Mkutano huu wa Bunge, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kujadili na
kuidhinisha Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali
katika mwaka wa Fedha 2016/2017.
Vilevile, Bunge limejadili na kutoa maoni na ushauri katika mwongozo wa
kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika mwaka wa Fedha, 2016/2017. Kipekee, naomba
nimshukuru
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango(Mb) na Naibu wake Dkt.
Ashatu Kachwamba Kijaji (Mb.) pamoja na Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara za
Kisekta kwa ufafanuzi mzuri walioutoa wakati wa kuhitimisha hoja hii. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza
Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao mizuri, maoni na ushauri ambao
Serikali itauzingatia katika kukamilisha maandalizi ya Mpango na Bajeti ya
mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Spika,
10.
Naomba
nami uniruhusu nitoe maelezo mafupi ya msisitizo katika maeneo machache yaliyopata
michango mingi kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja ya Serikali ya
mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo. Waheshimiwa Wabunge wengi
wamesisitiza kuhusu umuhimu wa Serikali kuongeza uwajibikaji katika ukusanyaji
wa mapato ya Serikali na kuimarisha udhibiti wa matumizi ya Serikali. Aidha, Waheshimiwa Wabunge wameishauri pia
Serikali kuweka kipaumbele cha ujenzi wa Reli mpya ya Kati, kujenga uchumi wa
Viwanda, kuanza na kusimamia ujenzi na Mitambo ya kuchakata gesi asilia (LNG)
na Kiwanda cha Mbolea Mkoani Lindi, kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme
Vijijini, ujenzi wa Bandari Mtwara, kutatua changamoto zinazowakabili Wakulima
na Wafugaji pamoja na Wachimbaji Madini.
Vilevile,
kuweka mikakati thabiti ya utekelezaji wa Miradi ya Sekta za Elimu, Afya, Maji
na huduma kwa wenye Ulemavu na pia kuzingatia utawala bora. Serikali inatambua kuwa maeneo haya ni muhimu
sana katika kujenga uchumi imara na endelevu na pia kuondoa umasikini. Hivyo, itazingatia sana ushauri huu mzuri
uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika,
11.
Naomba
nitumie fursa hii kumpongoeza Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa
umahiri mkubwa na umakini aliouonesha ikiwa ni mwanzo mzuri wa kuongoza
Serikali ya Awamu ya Tano. Mheshimiwa
Rais ameonesha kasi kubwa na dhamira ya dhati ya kuwatumikia Watanzania katika
kujenga uchumi imara, unaokuwa na endelevu.
Waheshimiwa Wabunge wengi watakubaliana nami kwamba Serikali ya Awamu ya
Tano katika kipindi chake cha mwanzo cha siku 100, imeonesha dhahiri nia ya dhati
ya kuhakikisha kwamba makusanyo ya mapato yetu yanaongezeka. Jitihada hizo za kuongeza makusanyo ya mapato
ya Serikali zimefafanuliwa vizuri kwenye Hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango. Serikali itaendelea na mikakati yake ya
kuongeza Mapato yake na kudhibiti mianya ya kukwepa kodi. Ni matumaini yangu kuwa Waheshimiwa Wabunge,
Wafanyabiashara na Wananchi wote wataunga mkono dhamira hiyo njema ya Serikali.
Mheshimiwa Spika,
12.
Kuhusu
matumizi, tayari Serikali imeanza kuchukua hatua thabiti za kudhibiti matumizi
yasiyo na tija katika Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea na Taasisi zote
za Umma pamoja Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Lengo la hatua zinazochukuliwa ni kuhakikisha
kwamba Serikali inasimamia kwa umakini matumizi ya fedha za Umma ili zitumike
ipasavyo kwa malengo yaliyokusudiwa.
Hatua hizi zitaimarishwa zaidi katika mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Spika,
13.
Kama
nilivyoeleza awali hoja nyingi za msingi zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge
kuhusu Mpango wa Taifa, zimefafanuliwa vizuri na Waheshimiwa Mawaziri wa
Kisekta na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango. Naomba niwaahidi kuwa tutazizingatia
katika mchakato wa maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017,
kwa kadri itakavyowezekana. Waheshimiwa
Wabunge watashirikishwa kikamilifu katika mchakato huo kupitia Kamati
mbalimbali za Bunge. Serikali
itafarijika sana kupata maoni na ushauri zaidi ili tuweze kuboresha mipango
yetu ya muda mfupi na muda mrefu.
III: SEKTA YA
KILIMO
Uzalishaji
wa Mazao ya Chakula 2014/2015 na Upatikaji wa Chakula 2015/2016
Mheshimiwa spika,
14. Hali ya chakula kwa mwaka 2015/2016
katika maeneo mengi ya nchi imeendelea kuwa ya kuridhisha kufuatia mavuno
mazuri yaliyopatikana msimu wa kilimo wa 2014/2015. Takwimu za Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
zinaonesha kuwa albaki kutoka msimu uliopita nchi ilikuwa na ziada ya chakula
licha ya kuwepo kwa maeneo machache ambayo hayakuwa na chakula.
Mheshimiwa
Spika,
14. Kutokana na uzalishaji wa mazao ya
chakula kwa msimu wa 2014/2015 kuwa Tani milioni 15.5 na mahitaji ya chakula
kwa mwaka 2015/2016 kuwa Tani milioni 12.9
hivyo nchi imejitosheleza kwa
chakula kwa ziada ya Tani milioni 2.5
sawa na asilimia 120. Napenda
kuwahakikishia Watanzania kuwa Serikali itaendelea kuhudumia maeneo yote yenye
uhaba wa chakula.
Mheshimiwa
Spika,
15. Pamoja na Taifa kuwa na ziada ya
asilimia 120 ya chakula, tathmini ya
hali ya chakula nchini inaonesha kuwa kuna Halmashauri 69 katika mikoa 18 nchini
yenye maeneo yenye dalili za upungufu wa chakula. Maeneo hayo yapo katika Mikoa
ya Dodoma, Shinyanga, Lindi, Singida,
Tabora, Arusha, Geita, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Tanga, Simiyu, Mwanza,
Morogoro, Iringa, Njombe, Mtwara, na Pwani.
Mheshimiwa
Spika,
16.
Ili kukabiliana na hali ya uhaba wa
chakula katika maeneo hayo, Serikali inaendelea kutoa chakula katika maeneo
hayo ambapo jumla ya Tani 23,871.6 za
chakula zilitengwa kwa ajili hiyo. Hadi kufikia tarehe 17 Januari, 2016, jumla
ya Tani 11,860.8 zilikuwa
zimechukuliwa toka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwenda kwenye
Halmashauri za Wilaya zenye upungufu wa chakula kwa ajili ya usambazaji. Natoa
wito kwa Halmashauri ambazo hazijachukua mgao wao kufanya hivyo mara moja ili
Wananchi katika maeneo hayo wasizidi kuathirika.
Mheshimiwa
Spika,
17.
Sambamba na utoaji wa chakula cha msaada, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula (NFRA) inaendelea kutoa mahindi katika maghala ya Songea na
Sumbawanga kwa ajili ya kuuzwa kwa wafanyabishara wa nafaka walioidhinishwa na
mikoa yenye uhaba wa Chakula. Lengo ni kuongeza upatikanaji wa chakula na
kukabiliana na kasi ya kupanda kwa bei ya vyakula katika maeneo hayo. Chini ya
utaratibu huo, vibali vimeshatolewa kwa wafanyabiashara wa Mikoa 17, vya kununua jumla ya Tani 77,166. Hadi kufikia tarehe 18
Januari, 2016 jumla ya Tani 56,817.5
kati ya Tani 64,817.3 zilizokuwa zimelipiwa kutoka NFRA tayari zilikuwa
zimechukuliwa.
Mheshimiwa
Spika,
18.
Ili kuongeza na kuimarisha uhakika na usalama wa chakula hapa nchini, Serikali
imelenga kujenga maghala 275 kwa awamu
katika sehemu zenye uzalishaji mkubwa wa zao la mahindi ambapo hadi sasa jumla
ya maghala 125 yanaendelea kujengwa
na kukarabatiwa katika maeneo hayo. Aidha, Serikali kwa kupitia Wakala wa Taifa
wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inaendelea kujenga maghala ya kimkakati kwa ajili
ya kuhifadhi akiba ya Taifa. Kwa sasa ghala moja lenye uwezo wa kuhifadhi Tani 5,000 limeshajengwa
Wilayani Mbozi Mkoani Mbeya. Aidha, Serikali imepata mkopo wenye masharti nafuu
kutoka Serikali ya Poland ambao utawezesha kujenga vihenge vya kisasa (silos) vyenye uwezo wa kuhifadhi Tani
160,000 na maghala yenye uwezo wa kuhifadhi Tani 90,000.
Mheshimiwa Spika,
19. Pamoja na hatua zinazochukuliwa na
Serikali, ninawataka viongozi wa Mikoa, Wilaya na atendaji katika Halmashauri zote Nchini kuwahamasisha
Wananchi kutumia vizuri mvua zinazonesha nchini kote kulima kwa bidii ili kuweza
kuvuna na kujiwekea akiba ya chakula cha kutosha kwa ajili ya kaya zao wakati
wote wa mwaka. Aidha, wawahamasishe wafanyabiashara na wadau wengine kusaidia Serikali
kuchukua chakula kutoka maeneo yenye ziada na kupeleka katika maeneo yenye
upungufu. Ni imani yangu kwamba tukizingatia maelekezo haya pamoja na juhudi za
Serikali zilizooneshwa, tatizo la uhaba wa chakula nchini litapungua, kama siyo
kumalizika kabisa.
IV: MIFUGO:
Hatua zilizochukulwa na
Serikali katika Kushughulikia Migogoro
ya Wakulima na Wafugaji;
Mheshimiwa
Spika,
20. Migogoro
ya ardhi hapa nchini ina sura nne; migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji,
mgogoro kati ya Wananchi na Wawekezaji; migogoro kati ya Wananchi na Serikali na
migogoro kati ya Mamlaka moja na Mamlaka nyingine ndani ya Serikali. Migogoro hii imeenea nchi nzima kutokana na
sababu mbalimbali ikiwepo kuongezeka kwa matumizi ya rasilimali ya ardhi.
21. Serikali kwa kushirikiana
na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi kwa
kutumia Sheria ya Ardhi ya Vijiji
Na. 5 ya mwaka 1999 na Sheria ya
matumizi ya Ardhi Na. 6 ya mwaka 2007, hadi kufikia mwezi Juni 2015 jumla ya
Vijiji 620 katika Wilaya 81 kwenye Mikoa 22 zimeweza kutenga Hekta Milioni
1.9 kwa ajili ya Wafugaji. Wito
wangu kwa Wananchi na Wadau wa Kilimo na Ufugaji nawaomba kutunza na kuendeleza
maeneo haya ili yaweze kutumika kwa mujibu wa malengo yaliyopangwa.
Mheshimiwa
Spika,
22. Nitumie fursa hii pia kulijulisha Bunge
lako Tukufu kuhusu hatua ambazo Serikali imechukua kukabiliana na migogoro ya
Wakulima na Wafugaji iliyotokea katika Mikoa ya Morogoro (Wilaya za Mvomero na
Kilombero) na Manyara (Wilaya ya Kiteto).
Katika kushughulikia tatizo hili, Jumla ya Vijiji 53 vimeainisha maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo
Kilimo na Ufugaji. Aidha, jumla ya
Mashamba Pori Manane (8) yameanishwa na orodha yake imewasilishwa kwa
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua za kufutiwa hati
miliki na hatimaye kufanya utaratibu wa kuyatumia kwa ufugaji. Ni matarajio
yangu kuwa maeneo haya yatapunguza kwa kiasi kikubwa matatizo ya uhaba wa
malisho hapa Nchini. Wito wangu niwatake
Viongozi wa Vijiji kusimamia vizuri matumizi ya maeneo yatakayotolewa kwa ajili
ya malisho ili tatizo hili la kukosa maeneo ya malisho lisijirudie tena.
Mheshimiwa
Spika,
23. Bado kuna mgogoro wa Wafugaji na
Wakulima katika Bonde Oevu la Kilombero ambao umetafutiwa ufumbuzi kwa kuweka
alama (branding) mifugo yote katika
eneo hili ambapo jumla ya Mifugo 52,780
ilipata usajili wa Wilaya. Aidha, jumla
ya Mifugo 24,586 imeondolewa katika
eneo la Bonde la Kilombero. Kwa
kuzingatia hatua zilizochukuliwa na Serikali Wananchi wanapaswa kufuata Sheria
na kuhakikisha Mifugo hairudi tena katika maeneo yaliyokatazwa na kwamba maeneo
haya yanahifadhiwa kwa mujibu wa Sheria.
Mheshimiwa
Spika,
24. Mgogoro wa Wafugaji na
Wakulima katika maeneo ya Kiteto ni wa muda mrefu na kwa bahati mbaya sana
umeleta madhara makubwa kwa maisha ya Wanadamu na uharibifu wa mali. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba
Tume iliyoundwa na aliyekuwa Waziri Mkuu (Mstaafu) Mheshimiwa Mizengo Peter
Pinda imekamilisha hatua muhimu ya kuleta maelewanao na maridhiano katika pande
zilizoathirika na mgogoro huo. Kwa sasa
hali imeendelea kuimarika na tunaendelea kufuatilia kuhakikisha inakuwa shwari
kwa muda wote.
25. Vilevile tarehe 29
Januari 2016 nimekutana na Viongozi wa Serikali, Halmashauri ya Wilaya na Chama
kutoka Wilaya ya Kiteto hapa Dodoma ambapo nilipata fursa ya kupokea taarifa ya
Tume niliyoitaja hivi punde. Nimeiagiza
Tume kuendelea na hatua iliyobakia ili kurejesha utulivu na amani kwa wananchi
wa Kiteto. Hata hivyo, nimepanga kufanya ziara Wilayani Kiteto katika siku chanche
zijazo ili niweze kukutana na Wananchi walioathirika na mgogoro huu na ikiwa ni
pamoja na kujionea hali halisi Wilayani Kiteto.
Wito wangu kwa ndugu zangu wa Kiteto ni kuwaomba waendelee kuvumilia
wakati jitihada za Serikali katika kutatua migogoro hiyo inaendelea.
V: UTEKELEZAJI WA ELIMU MSINGI BILA MALIPO
Mheshimiwa Spika,
26. Tangu Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe
Magufuli atoe maaelezo ya utekelezaji wa elimumsingi bila malipo, kumekuwa na
umuhimu wa kutoa elimu na ufafanuzi zaidi juu ya utekelezaji wa agizo la elemu bila
malipo kwa Watanzania kuanzia darasa la awali hadi Kidato cha Nne katika Shule
za Umma. Hii ni hatua ya Serikali katika
kuhakikisha uwepo wa fursa ya elimu bora kwa wote kwa kuwapunguzia mzigo wazazi
na walezi kugharamia au kuchangia upatikanaji wa elimumsingi. Katika mpango
huu, Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa mwanafunzi atasoma kuanzia darasa la
awali hadi kidato cha Nne bila ya wazazi na walezi kulipa ada ya shule, gharama
za mitihani na michango mbalimbali. Hata hivyo, yapo majukumu ambayo
yataendelea kutekelezwa na wazazi na walezi ambayo ni pamoja na kununua sare za
shule na michezo, madaftari, kalamu na chakula kwa wanafunzi wa shule za kutwa.
Maeneo mengine ni kulipia nauli ya kwenda na kurudi shule, na mahitaji mengine
kama kununua godoro, shuka na vifaa vya usafi binafsi. Mzazi au mlezi ana
wajibu wa kugharamia matibabu ya mtoto wake.
Mheshimiwa
Spika,
27. Napenda nitumie nafasi hii kuwaomba
Waheshimiwa Wabunge wote tushirikiane katika juhudi za kuunga mkono uamuzi wa
Serikali kuhusu elimu bila malipo.
Aidha, nawaomba wote kwa ujumla wetu kushirikiana kuwaelimisha Wananchi
wetu kuhusu utaratibu huu na wajibu wa kila mmoja wetu kama Mzazi/Mlezi,
Serikali na jamii kuhusu utekelezaji wa zoezi hili. Nia yetu ni kuhakikisha Watanzania wanapata
fursa ya kupata elimu bora kwa mtoto mwenye umri wa kwenda Shule na wote
walioko katika Shule za Msingi na Sekondari.
Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kama tulivyo kwisha sema
suala la ada elekezi inafanyiwa kazi na ikikamilika Wananchi watajulishwa
kuhusu utaratibu huo.
Mheshimiwa
Spika;
28. Katika kutekeleza
mpango huu, Serikali imetenga fedha shilingi Bilioni 131.4 kuanzia mwezi Disemba 2015 hadi Juni, 2016, kuhudumia
wanafunzi wa bweni kwa chakula, kufidia gharama za ada za mitihani, ada ya
shule na kutoa fedha za uendeshaji wa shule (Capitation Grants). Aidha, kupitia Waraka wa Elimu Na. 5 wa mwaka
2015 Serikali imefuta michango yote
iliyokuwa inachangishwa shuleni kwa idhini ya Kamati na Bodi za Shule.
Mheshimiwa Spika,
29. Tunatambua katika utekelezaji wa zoezi
hili zipo changamoto zilizojitokeza. Kwa
mfano, baadhi ya shule zenye wanafunzi wachache kupata fedha kidogo sana kwa
kuwa ugawaji wa fedha unazingatia idadi ya wanafunzi. Lakini pia zipo changamoto katika kutoa
chakula cha mchana kwa Wanafunzi wa kutwa na uendeshaji wa Hosteli ambazo
wazazi na walezi au jamii walikuwa wanachangia fedha za chakula. Serikali
inaendelea kuzifanyia kazi
changamoto hizo zilizojitokeza katika utekelezaji wa mpango huu ikiwemo uelewa
wa jamii na wadau kuhusu mpango mzima kwa ujumla wake.
VI: HUDUMA YA MIKOPO KWA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
Mheshimiwa Spika,
30. Serikali imeendelea kutoa huduma ya
mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2015/2016 kwa kuzingatia
Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Namba 9 ya mwaka 2004
(Kama ilivyorekebishwa), Kanuni za Utoaji Mikopo za mwaka 2008, na Mwongozo wa
utoaji Mikopo na Ruzuku kwa mwaka wa masomo 2015/2016. Hadi kufikia mwishoni
mwa Januari 2016, Serikali ilikuwa imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 207.9 kwa wanafunzi 122,786 wa elimu ya juu, wakiwemo
wanafunzi wa mwaka wa kwanza 53,850 ambao
ni Asilimia 98.9 ya wanafunzi 55,254 walioomba mikopo hiyo.
Mheshimiwa
Spika,
31. Ili Taifa liendelee kuwa na wataalamu wa
kutosha katika nyanja muhimu, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele cha kutoa
mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wanaodahiliwa katika programu za kipaumbele ikiwemo Sayansi za Tiba, Ualimu wa Sayansi na
Hesabu, Uhandisi wa Mafuta na Gesi,
Uhandisi Umwagiliaji, Sayansi za Kilimo, Wanyama na Ardhi. Aidha, Serikali inaendelea kufanyia
kazi mikakati ya kuimarisha urejeshaji wa mikopo pamoja na kuwa na vyanzo
endelevu vya kupata fedha za kumudu ongezeko la wanafunzi wenye mahitaji ya
mikopo.
VII: HALI YA USALAMA NCHINI
Mheshimiwa Spika,
32. Hali ya
usalama katika Nchi yetu kwa ujumla ni shwari.
Hata hivyo, katika kipindi hiki
nchi yetu imekuwa ikikabiliana na changamoto ya
ongezeko kubwa la Wakimbizi hususan katika Mkoa wa Kigoma. Kambi zetu zilizoko
mikoa ya Kigoma, Katavi, Tabora na Tanga zinahifadhi wakimbizi wapatao 218,895
kutoka mataifa ya
Burundi (156,377), Congo-DRC
(62,176), Somalia (150) na
Mataifa Mchanganyiko (192) kutoka
nchi za Rwanda, Uganda,
Sudani ya Kusini
na Ethiopia. Kwa ujumla katika
kipindi hiki wamepokelewa wakimbizi zaidi ya 122,267 kutoka Burundi. Aidha,
hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2015
kambi mpya ya wakimbizi ya Nduta
imepokea wakimbizi 38,994 wengi kati yao wamehamishiwa kutoka Kambi ya
Nyarugusu na wachache wakiwa wameingia
moja kwa moja kutokea Burundi.
Mheshimiwa Spika,
33. Kufuatia ujio wa
wimbi kubwa la wakimbizi toka Burundi
kumejitokeza matukio ya uhalifu wa kutumia silaha za moto ndani na nje
ya kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu.
Aidha, kutokana na upekuzi
na ukaguzi kwa wakimbizi unaofanywa kwa pamoja na
vyombo vya dola sanjari na taarifa za ki-intelijensia imebainika kuwepo kwa
askari waasi waliokimbia pamoja na raia wa kawaida ambao wanajaribu kuwashawishi vijana kujisajili ili
kujiunga na vikundi vya waasi. Nitoe wito kwa wananchi na wakimbizi
kushirikiana na vyombo vyetu vya usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu, hususan
umiliki haramu wa silaha za moto kwenye Makambi na katika maeneo mbalimbali.
VIII: MPANGO ENDELEVU WA USAFI WA MAZINGIRA NCHNI,
Mheshimiwa Spika.
34. Mtakumbuka kuwa Mheshimiwa Rais Dkt.
John Pombe Magufuli, aliamua maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru ya terehe 9
Desemba, 2015 yafanyike kwa kufanya usafi wa mazingira katika maeneo ya Umma na
maeneo yanayowazunguka. Kwa ujumla
Wananchi, Taasisi za Umma na Binafsi ziliitikia agizo hilo na kushiriki
kikamilifu katika zoezi hilo. Nichukue
fursa hii kuwapongeza kwa dhati Wananchi, Taasisi za Umma na Binafsi wote kwa
kushiriki katika zoezi hilo kikamilifu. Mlionesha moyo wa uzalendo na ari kwa
nchi yenu. Nawapongeza sana!
Mheshimiwa Spika,
35. Usafi ni dhana muhimu katika kulinda
afya za binadamu na kudhibiti magonjwa mbalimbali ya mlipuko ikiwemo
kipindupindu. Ili kufanikisha lengo hili, kunahitajika juhudi za makusudi na za
pamoja katika usimamizi wa Sheria, Kanuni na Taratibu tulizojiwekea. Hivyo, Serikali imeamua kulifanya zoezi la
usafi wa mazingira kuwa endelevu. Kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Serikali
imetoa Waraka unaoelekeza kuwa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi iwe siku maalum
ya kufanya Usafi wa Mazingira.
Mheshimiwa Spika,
36. Napenda kuendelea kusisitiza katika kila
ngazi yaani Viongozi na Wananchi kutimiza wajibu wako kwa kuhakikisha zoezi
hili linakuwa endelevu. Aidha, napenda kuwahimiza Viongozi wa Mkoa, Wilaya na
Halmashauri kusimamia usafi wa mazingira katika maeneo yao ya utawala zoezi ambalo
litakuwa linafanyika kila Jumamosi ya mwisho wa Mwezi. Kila Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya Nchini awe na mikakati ya kudumu ya usafi ikiwa ni pamoja
kuhakikisha kuwa kuna Sheria Ndogo za usafi wa mazingira na zinatekelezwa
ipasavyo. Aidha, Halmashauri zote Nchini zihakikishe kuwa uchafu uliokusanywa
katika maeneo mbalimbali unazolewa na kupelekwa katika maeneo mahususi ya
dampo. Simamieni kikamilifu Wakandarasi
waliopewa zabuni hizo na kuona wanatimiza wajibu wao kikamilifu.
Mheshimiwa Spika,
37. Kama tulivyoona Usafi wa mazingira ni
jukumu la kila Mwananchi na linapaswa kuwa endelevu. Rai yangu kwa Watanzania wote ni kujenga
tabia ya kuhakikisha kuwa mahali pa kazi na mazingira yanayowazunguka yanakuwa
safi wakati wote. Kufanya hivyo, kutasaidia kuimarisha usafi wa mazingira na
kuboresha afya. Hali kadhalika kupunguza
mlipuko wa magonjwa yakiwemo Kipindupindu.
38. Wito wangu kwa Wananchi ni kuona kuwa
zoezi la usafi ni la kila mmoja wetu na kuepuka kuchafua mazingira kwa makusudi
ikiwemo kuepuka tabia za kutupa taka hovyo wanapokuwa katika vyombo vya usafiri
na pia kutofanya biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa ili kuzuia kutupwa taka hovyo. Watendaji wa Mitaa na Kata na Vijiji kutimiza
wajibu wao wa kuhakikisha maeneo wanayoyasimamia yanakuwa katika hali ya
usafi. Nitumie fursa hii kuwahimiza
Wananchi, Taasisi na Jumuiya zote kuhakikisha wanaweka mazingira katika hali ya
usafi na pia kushiriki katika siku ya usafi kama iliyopangwa na Serikali.
IX: UHUSIANO WA KIMATAIFA
Mheshimiwa
Spika,
39. Nchi yetu imeendelea kuwa kivutio
kikubwa katika mahusiano baina ya Nchi na Nchi, Jumuiya za Kikanda na
Kimataifa. Hii inatokana na Viongozi
wetu ambao wamekuwa katika mstari wa mbele kudumisha mahusiano yetu katika
Medani za Kimataifa. Yapo mambo mengi
yaliyofanyika na yanayo endelea kufanyika kama mwendelezo wa kudumisha
ushirikiano katika Jumuia hizi za Kikanda na Kimataifa.
Mheshimiwa
Spika,
40. Kutokana na juhudi za Viongozi wetu
kutangaza Nchi yetu Kimataifa, ni hivi karibuni tu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa
Serikali ya Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliteuliwa na
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Ban Ki-moon kuwa mmoja wa Wenyeviti wa
jopo la ushauri la ngazi ya juu kuhusu Afya ya Mama na Mtoto (Every Woman, Every Child) Duniani. Hii
ni heshima kubwa kwa nchi yetu kwa kuwa itaiweka Tanzania
kuwa miongoni mwa mataifa yenye kuheshimika duniani. Aidha, uteuzi huu
ni chachu ambayo inaleta matumaini mapya katika kukabiliana na changamoto za afya ya mama na mtoto, hususan katika nchi
zinazoendelea kama Tanzania. Nitumie
fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa uteuzi huo.
Tunamuombea heri na baraka tele katika kutekeleza jukumu hilo kubwa la
Kimataifa kwa maendeleo ya watu wetu.
X: KUIMARISHA
UTENDAJI SERIKALINI NA MAADILI
Mheshimiwa
Spika,
41. Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa
na Chama cha Mapinduzi imedhamiria kurejesha nidhamu na maadili ya Watendaji wa
Serikali na Watumishi wa Umma katika kutoa huduma mbalimbali kwa Wananchi.
Katika kuhakikisha Watumishi wa Umma na Watanzania wote wanafanya kazi,
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
amekuja na kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”. Tafsiri ya
falsafa hii ni kuwataka Watanzania wote katika nafasi mbalimbali walizopo
kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha na vitendo vya uzembe, urasimu na kutenda kazi kwa mazoea.
42.
Aidha, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 chini ya Ibara ya 22 inaainisha kuwa,
kila Mtu anayo haki ya kufanya kazi. Vilevile, Ibara ya 25 inafafanua kuwa kufanya kazi ndiyo njia pekee ya
kumwezesha Mtanzania kupata utajiri na ndilo chimbuko la ustawi wa wananchi na
ni kipimo cha utu.
Wakati akihutubia Mkutano wa kwanza wa Bunge
lako Tukufu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa maneno yake alisema,
napenda kunukuu:-
“Serikali
nitakayounda, nataka iwe inawahudumia Wananchi kwa haraka na sio kuwasumbua
sumbua na kuwazungusha. Natoa rai kwa
Watumishi wa Serikali, hasa ambao ni wazembe na wavivu, kujiandaa. Wamevumiliwa
kwa muda mrefu sasa basi. Kwa sababu Watumishi wa aina hiyo hawatavumiliwa katika
Serikali nitakayoiongoza. Lugha za “Hiyo
ni changamoto tutaishughulikia” au “Mchakato
unaendelea” hazitavumiliwa katika Serikali ya Awamu ya Tano. Mimi nataka watu wa Kazi tu. Hatuwezi kulea watu
ambao wanalipwa mishahara lakini hawafanyi kazi wanazotakiwa kufanya, au
wamegeuza Ofisi za Umma kuwa ni mahala pa kuchuma bila kufanya kazi.” mwisho
wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika,
43.
Ili kutekeleza
maneno ya Mheshimiwa Rais na kuhimiza matakwa ya Kikatiba, kila Mtanzania
anapaswa kushiriki na kujituma kwa uaminifu katika kazi halali za uzalishaji
mali. Aidha, kila Mwananchi anapaswa kuwa na nidhamu ya kazi na kuhakikisha
anafikia malengo yaliyowekwa. Nitumie fursa hii pia kuwakumbusha Watumishi wa
Umma kuwa wamepewa dhamana ya kuwahudumia Wananchi kwa niaba ya Serikali. Hivyo wanawajibika kuhakikisha wanawahudumia
Wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na kwa taaluma zao. Ni lazima wahakikishe kuwa
wanatatua kero za Wananchi. Sio sahihi
wananchi kuwasilisha kero zao kwa viongozi wa ngazi za kitaifa hasa wakati wa
ziara ilihali viongozi wa mikoa na wilaya wapo katika maeneo hayo kwa wakati
wote.
44.
Tunatambua kuwa wapo Watumishi wanaotekeleza vyema majukumu yao. Lakini pia wapo
Watumishi ambao hawazingatii maadili ya kazi zao na pia wanafanya kazi kwa
uzembe. Serikali haitaacha kuchukua hatua za nidhamu kwa watumishi wote wasio
zingatia kikamilifu sheria, kanuni na taratibu katika Utumishi wa Umma. Aidha, kwa kuzingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais,
Viongozi na Watumishi wote wa Umma lazima tufanye kazi kwa kuzingatia weledi na
kujiamini. Kila Mtu
anapaswa kujitathmini kama dhamana aliyopewa anaitendea haki.
Mheshimiwa Spika,
45.
Huu
sasa ni wakati wa kufanya mabadiliko ya dhati katika utendaji na uadilifu. Kwa
maana hiyo napenda kusisitiza mambo yafuatayo kwamba:-
(i)
Kila Kiongozi na Mamlaka ya nidhamu ni
lazima kuwajibika kusimamia Utendaji na Maadili ya Kazi. Hatua za kinidhamu
zichukuliwe kwa wakati na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za
Utumishi. TUSIONE HAYA HATA MARA MOJA, CHUKUENI HATUA.
(ii)
Wananchi
wahudumiwe ipasavyo na kwa weledi, haki, uadilifu na heshima. Mambo haya
yakizingatiwa hakuna mwananchi atakayesafiri kutoka kijijini, Wilayani au
Mkoani kutafuta huduma Makao Makuu ya Wizara, Ofisi ya Waziri Mkuu au IKULU.
(iii)
Madawati ya malalamiko yawepo katika Ofisi
za Umma. Aidha, tayari maelekezo yametolewa ya Watumishi wa Umma wazingatie
utaratibu wa kuvaa vitambulisho vyenye majina yao kwa urahisi wa Wananchi
kuwatambua wanapowahudumia. AGIZO HILI LITEKELEZWE.
Mheshimiwa Spika,
46.
Ni
kweli kwamba, Mheshimiwa Rais ametumia dhana ya “kutumbua jipu” kama dawa ya kusimamia uwajibikaji hasa katika wale
wenye dalili ya kukosa maadili ya Utumishi wa Umma. Tafsiri ya dhana hii ya “Kutumbua jipu” inalenga katika
kuwarejesha Watumishi wa Umma na walioko Serikalini katika mstari mzuri wa
utendaji. Nitoe wito kwa Waheshimiwa
Wabunge wote kama tulivyo na kwa umoja wetu tuumunge mkono Mheshimiwa Rais
katika vita hii kubwa ya “Kutumbua
Majipu”. Tukiwa pamoja na kwa
kushirikiana tutaweza kuibadilisha Nchi yetu kuwa Nchi ya maadili na yenye sifa
ya juu katika utendaji wa Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa Spika,
47.
Aidha, naomba
nisisitize kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Magufuli inaongozwa na Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu za Nchi. Vilevile inaheshimu
na kuthamini haki za Watumishi wa Umma wa ngazi zote na inatambua mchango
mkubwa unaotolewa na Watumishi wa Umma katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa
Taifa. Kamwe, Serikali haitamwonea Mtumishi yeyote wala kumnyanyasa. Lakini pia
haitamvumilia Mtumishi mzembe na asiye timiza wajibu wake. Serikali itaendelea
kuchukua hatua za kurejesha nidhamu kwa Watumishi wa Umma ili kuwezesha Nchi
yetu kuwa na Utumishi wenye kuzingatia uadilifu na uliotukuka.
XI: HITIMISHO.
Mheshimiwa Spika,
48.
Uzoefu
nilioupata katika muda mfupi tuliokaa pamoja hapa Bungeni, nimegundua kuwa tuna
Waheshimiwa Wabunge mahiri waliobobea katika nyanja mbalimbali. Wapo wasomi wa
ngazi zote, Wazee kwa Vijana ambao wana uzoefu na Utaalam mkubwa. Ni imani yangu
kuwa tutatumia utaalam na uwezo mkubwa tulionao katika kuijenga Nchi yetu na
kuwasaidia Watanzania kutoka hapa tulipo hadi hatua ya mbele katika kuleta
maendeleo. Wananchi waliotuchagua wanatutegemea. Nawaomba tutangulize uzalendo
katika kila jambo tufanyalo kwa manufaa ya Taifa letu na watu wake. Tufike
mahali ambapo kwa elimu, busara na hekima tulizonazo kuacha kabisa ushabiki wa kisiasa
badala yake tutizame mbele katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Mheshimiwa Spika,
49.
Napenda
kuhitimisha Hotuba yangu kwa kurejea tena nilivyosema hapo awali kwamba, baada
ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu kwa mafanikio makubwa, kazi kubwa iliyo mbele yetu
ni kuijenga Nchi yetu kwa umoja na mshikamano. Nawaomba tuweke maslahi ya
Watanzania na Taifa letu mbele. Tudumishe amani na utulivu. Tupuuze sera zozote
za kudhoofisha utaifa wetu kama Watanzania na kutugawa kwa misingi yoyote ile,
iwe ya kikabila, imani za dini, rangi au kwa itikadi za kisiasa. Dhamira yetu
sote iwe ni kukuza uchumi wa Nchi yetu na kuondoa umaskini ili kuwaletea
Wananchi wetu maendeleo na maisha mazuri.
50.
Ni
jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa Tanzania inapiga hatua mbele.
Tufanye kazi kwa bidii kuunga mkono kaulimbiu yetu ya “Hapa ni Kazi Tu”. Aidha
tutumie juhudi, maarifa na ubunifu zaidi katika kila jambo. Mimi naamini kuwa
kwa ushirikiano katika Bunge hili na Wananchi kwa ujumla tutaweza kutimiza
matarajio ya Wananchi waliotuchagua na matarajio ya Watanzania wote.
Mheshimiwa
Spika,
51.
Naomba nitumie
nafasi hii tena kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha mkutano huu. Nikushukuru
wewe Mheshimiwa Spika na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri na kwa weledi mkubwa. Kipekee niwashukuru Wenyeviti wa Bunge ambao wamekalia
kiti kwa mara ya kwanza lakini kwa weledi mkubwa, Hongereni sana!!.
Mheshimiwa
Spika,
52.
Nitumie nafasi hii kumshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi
wake wote kwa kazi nzuri ya kuhakikisha mkutano huu unakamilisha shughuli zake
kama ilivyopangwa. Niwashukuru Wataalam wote wakiwemo Waandishi wa Habari kwa
kazi nzuri waliyofanya kufanikisha Mkutano huu.
Mheshimiwa
Spika,
53.
Nimalizie kwa kuwatakia wote safari njema mnaporejea kwenye
maeneo yenu ya kazi na katika majimbo yenu.
Ninaamini kwamba, Mwenyezi Mungu atatulinda na kutuweka salama sote kama
tulivyo hadi kukutana tena katika Mkutano ujao.
Mheshimiwa
Spika,
54.
Baada ya kusema hayo, naomba sasa kutoa Hoja kwamba, Bunge
lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 19 Aprili, 2016 saa
3:00 asubuhi litakapokutana katika
Mkutano wa Tatu kwenye Ukumbi huu
hapa Dodoma.
Mheshimiwa
Spika,
55.
Naomba kutoa Hoja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni