Vijana
wanatakiwa kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa bidii kama njia pekee ya
kujikwamua na umasikini.
Hayo
yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Mhe. Said Mtanda
(Mb.) jana wakati kamati hiyo ilipokuwa
ikikagua miradi inayoendeshwa na vikundi vya vijana katika Halmashauri ya
Manispaa ya Temeke vilivyopata mikopo kutoka katika Mfuko wa Maendeleo ya
Vijana unaoratibiwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Mhe.
Mtanda alisema kuwa ajira za maofisini haziwezi kutosheleza kila kijana kutokana
na ukweli huo ni wakati wa vijana
kupambana na hiyo changamoto kwa njia ya kujiajiri kwa kubuni miradi ya
kuwatengenezea kipato hali itakayowakwamua katika umaskini.
“vijana
msiogope kuthubutu siyo lazima kuanza na mradi mkubwa anza na huo huo mdogo ipo
siku utakuwa mradi mkubwa hata mbuyu ulianza kama mchicha”. Alisema Mhe.
Mtanda.
Miradi
iliyokaguliwa na Kamati hiyo ni pamoja na mradi wa kilimo cha matikitimaji,
mapesheni na ufugaji kuku unaoendeshwa na Kikundi cha Vijana kijulikanacho kama
Sokoine Youth Development kilichopo
kata ya Somangila, Kigamboni.
Kikundi
kingine kilichokaguliwa ni kikundi cha vijana waliohitimu na walioko vyuo vikuu
kijulikanacho kama African Legends kilichopo
Kigamboni; kikundi hiki
kinachojishughulisha na mgahawa pamoja na maswala ya teknolojia ya habari na
mawasiliano.
Aidha,
Kamati hiyo ilikagua kikundi
cha Vijana cha Waungwana Youth Family
kinachojishughulisha na kazi za saluni pamoja na muziki; kikundi hiki kiko
katika kata ya Sandali.
Mhe.
Mtanda aliwakumbusha vijana umuhimu wa kujiunga katika vikundi vya vijana ili
watambulike na wajiunge katika SACCOS za vijana katika Halmashauri wazoishi ili
iwe rahisi kukopa katika Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Naye
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Juma Nkamia (Mb.)
alisema kuwa Wizara imejipanga kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi na
imekuwa ikitoa elimu ya ujasiriamali na stadi za maisha zoezi ambalo ni
endelevu kwani hadi sasa wataalamu wanazunguka katika mikoa mbalimbali kwa
ajili ya kazi hiyo.
Mhe.
Nkamia alisema kuwa Wizara itaendelea kuwezesha vikundi vya vijana ambavyo
tayari vina miradi ili iweze kukua zaidi na kuwa miradi mikubwa yenye uwezo wa
kutengeneza ajira kwa vijana wengine.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa SACCOS ya Vijana ya Temeke, Bw Swaka Abbas ambapo
ndiko mikopo ya vikundi hivyo ilikopitishiwa aliishukuru Kamati hiyo kwa
kuwatembelea na kuwatia moyo. Pia aliishukuru
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na Halmashauri ya
Manispaa ya Temeke kwa ushirikiano wanaoupata katika kazi zao za kutokomeza
umaskini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni