*Ni kuhusu kubeza juhudi za
Serikali Kagera
*Wasomi wamshukia, wamtaka
aache siasa
Na Mwandishi wetu
WADAU mbalimbali wamempongeza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwa
muwazi kwa wananchi wake wakati wanapohitaji misaada mbalimbali wakati wa
majanga.
Wametoa kauli hiyo leo jijini
Dar es salaam wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hizi kueleza kauli ya
hivi karibuni ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye
amekaririwa akidai kuwa kauli za Rais mkoani Kagera ni za hatari.
Wamesema kuwa baadhi ya
Watanzania wamezoea kupewa ahadi ambazo kwa wakati mwingine ni vigumu
kutekelezeka na sasa watu kama Mbowe bado wako kwenye mtazamo huo.
Wameongeza kuwa Rais Magufuli
amekuwa siku zote mkweli, jambo ambalo baadhi ya watu wasiopenda ukweli
wanapotosha kauli zake kwa kutaka kuwachonganisha wananchi na Rais wao ambaye
amekusudia kuwaletea wananchi maendeleo.
Rais Magufuli akiwa Kagera hivi
karibuni alisisitizia msimamo ambao si mpya, umekuwa msimamo wake na wa
Serikali tangu yalipotokea maafa ya tetemeko la ardhi mkoani humo kwamba
Serikali itasaidia lakini haitaweza kumjengea nyumba kila mtu.
“Baadhi ya wanasiasa na
viongozi wamekuwa wakitoa kauli zenye kupotosha na kubeza hotuba ya Rais Magufuli mkoani Kagera
jambo ambalo sio zuri na sio ukomavu wa kiasa” walisema.
Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu
cvha Dar es Salaam, Dkt Bashiru Ally amesema kuwa katika mfumo wa siasa huru
kuna kutofautiana mitazamo kati ya wananchi ,Serikali na viongozi wa siasa
lakini ni wazi kuwa Rais alisimama katika msimamo wa Serikali yake na uwezo wa
kutekeleza ahadi zake.
Alisema kuwa Rais Magufuli
alikuwa na maana nzuri ya kukabiliana na majanga nchini inategemea uwezo wa
nchi na mshikamano wa wananchi na huo ni ukweli ambao wengi hawakupenda
kuusikia.
Dkt. Bashiru Ally alisema kuwa
kwa janga la Kagera kulikuwepo mshikamano wa Serikali katika ngazi zote,
wananchi na wadau mbalimbali walishiriki kwa namna moja ama nyingine
kukabiliana na janga hilo.
“Wito wangu ni kuwataka
wanasisa kujifunza kutokana na majanga badala ya kutoa kauli tatanishi na zenye
kubomoa mshikamano wa wananchi, bali wanatakiwa
kukosoa bila kubeza, kupotosha kwa namna ni ya kungwana,” alisema Dkt
Bashiru
Kwa upande wake Dkt. Benson
Bana kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema kuwa watu wanatafsiri vibaya
maneno ya Mhe. Rais aliyoyaongea Mkoani Kagera hivi juzi.
“Mheshimiwa ameongea ukweli kwa
sababu ni sahihi kuwasaidia watu wengi kwa pamoja kuliko kumsaidia mtu mmoja
mmoja,” alisema.
Aliongeza kuwa hakuna haja ya
kuwa na wasiwasi juu ya lugha za Mhe. Rais kwani lugha zake hazina ubabaishaji
ni za kweli na ziko moja kwa moja, hao wanaomuongelea vibaya ni wale wenye
lengo la upinzani tu na sio maendeleo ya Taifa.
Ameongeza kuwa kwa upande wake pamoja
na wananchi wenye mapenzi ya kweli wamemuelewa Mhe. Rais na ndio maana walikuwa
wakimpigia makofi wakati akiongea kule Kagera.
”Mimi nilikuwepo mkoani Kagera
na hotuba za mheshimiwa zote nilizisikiliza kwa makini ndio maana nasema wanye
nia mbaya na Rais ndio wanaoongea mabaya juu
yake kwani mbona alivyoongelea suala la kupunguza umeme hawakusema
chochote?” alihoji Dkt. Bana.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa
Chama cha United Democratic Party (UDP) John cheyo amewataka Watanzania
kutotegemea serikali kwa kila kitu pindi wanapopatwa na majanga.
Alisema kuwa lengo la
Mheshimiwa Rais Magufuli ni kutaka Watanzania kujenga utamaduni wa kujitegemea
pindi wanapofikwa na majanga mbalimbali na ndio maana alitaka kujua juhudi zao
kabla ya kuomba msaada wa Serikali.
Profesa Haji Semboja alisema
kuwa kauli ya Rais ilikuwa ni kuwahimiza watu wa Kagera ambao anajua wana uwezo wa mambo mengi ya kulima
mazao mbalimbali kama vile mazao ya chakula na biashara ikiwemo ndizi na kahawa
ambayo yanaweza kuwapatia chakula cha kutosha wananchi wa mkoa huo.
Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha
Diplomasia nchini Dkt. Bernad Achiula amesema kuwa baadhi ya wananchi wamepokea hotuba ya Rais John Magufuli kwa mtazamo
tofauti, lakini ni dhahiri hakuna nchi yeyote duniani ambayo inahudumia kila mwananchi
katika majanga ya kiasili yanayotokea.
“Wajibu wa Serikali katika nchi
yeyote ni kujenga na kuboresha
miundombinu mbalimbali iliyotokea ikiwemo barabara, hospitali, shule,
malazi ya muda kwa waadhirika, madawa, miundombinu ya umeme, maji kwa waathirika
hatua inayolenga kuwapa pole waathirika hao.
Alisema kuwa hatua hizo
zinalenga kutoa huduma kwa wananchi wengi kuliko kutoa msaada kwa mtu mmoja
mmoja. Alisema wanaotaka kumlaumu Rais basi wangemlaumu kama angekuwa Serikali
yake haijatoa huduma hizo muhimu.
Alipoulizwa kuhusu kauli hizo
za Mbowe, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO ambaye pia ndiye Msemaji Mkuu
wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi alisema lugha ya Rais na Serikali kwa ujumla
kuhusu maafa ya Kagera na mengine yaliyotokea nchini haijawahi kubadilika wala
kutetereka.
“Rais na Serikali yake kwa
ujumla wamekuwa wazi katika hili na itaendelea kuwa wazi kwamba kama Taifa
hatuna raslimali za kumsaidia kila mwathirika wa tetemeko la Kagera kwa
kumfanyia kila kitu.
Serikali ilitibu majeruhi wote
bure, ilisaidia kifuta machozi kwa familia zote zilizopoteza ndugu zao,
ilisaidia waathirika kupata huduma za kibinadamu kama dawa, ushauri wa
kisaikolojia, vyakula na mavazi na maturubai kwa makazi ya muda na inaendelea
kujenga miundombinu kama shule, zahanati na barabara,” alisema.
Dkt Abbas akasisitiza: “Mbowe
atafute tu ajenda nyingine. Nilikwenda Kagera na kukaa kwa wiki mbili baada ya
tetemeko kutokea ambapo nilibahatika kuzungumza na waathirika mijini na
vijijini; hakuna kati yao popote aliyekuwa anasema Serikali itamjengea nyumba
au kumsaidia kila kitu. Kwa hiyo ujumbe wa Rais ulieleweka tangu mwanzo na hata
sasa.”
Ameongeza kuwa Serikali
imesaidia kaya maskini kwa kuwapatia saruji na mabati kwa ajili ya ujenzi wa
nyumba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni