![]() |
Mganga Mkuu wa
Serikali akizungumza na wataalamu wa Afya katika moja ya mikutano yao(Picha
kutoka maktaba)
|
Na: Mwandishi Wetu
Serikali
imesema itachukua hatua kali ikiwemo kuanza kuwashtaki wavamizi wote wa taaluma
ya tiba ya viungo vya mwili ijulikanayo kama ‘fiziotherapia’ baada ya kubaini
uwepo wa wimbi kubwa la watu wasio na sifa ya kuhudumu tasnia hiyo.
Hayo
yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Muhammad Bakari Kambi, wakati
akifungua mkutano wa mwaka wa wanachama wa Fiziotherapi nchini (APTA) Dar es
Salaam leo.
Alisema
serikali kupitia wizara ya Afya ipo mbioni kukamilisha mchakato wa kutunga
sheria mpya itakayohusika kudhibiti wavamizi na wachafuzi wa tiba hiyo muhimu
ambao wametapakaa maeneo mbalimbali nchini baada ya ile ya awali kuonyesha
baadhi ya mapungufu.
“Muswada
wa sheria mpya ambayo tuko mbioni kuikamilisha itatambua rasmi taaluma hii
muhimu na nyinginezo kama taaluma ya meno, na sayansi za afya shirikishi chini
ya bodi itakayoundwa ili kudhibiti mwenendo wake hatua kwa hatua,” alisema Profesa
Kambi.
Aidha,
aliwataka mafiziotherapia waliopo nchini kote wapatao 350 kuonyesha mshikamano
wao kwa kujiunga pamoja ndani ya APTA ili kurahisisha utatuzi wa changamoto
zinazowahusu, kukabiliana na mianya ya uchafuzi wa taaluma hiyo na kuiwezesha
serikali kuwafikia kwa urahisi.
Pamoja
na mambo mengine, Mganga Mkuu aliwakumbusha kufanya kazi yao kwa kuzingatia
maadili, huku akisisitiza kuwa kinyume chake wataripotiwa kwa njia yoyote
ile..kwani dunia ya leo haina siri na inakwenda kiteknolojia zaidi hasa kwenye
eneo la upashanaji habari.
“Msikubali
mmoja wenu awachafue toeni taarifa tuchukue hatua mara moja, fanyeni kazi zenu
kwa weledi kumbukeni mpo kwenye nchi inayokua kwa kasi kiteknolojia mkiharibu
mtakutana na wanasheria wengi mitaani wanaotafuta kesi, na bado mtarekodiwa na
taarifa zenu kusambazwa mitandaoni,” alisema.
Kwa
upande wake, Rais wa APTA, Remla Shirima, alisema taaluma hiyo iliyoanzishwa
tangu mwaka 1948 hadi sasa ina wafiziotherapia 350 tu waliosajiliwa huku
ikikabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo wataalamu na vifaa tiba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni