JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
Simu: 255-22-2114512,
2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz
Faksi: 255-22-2113425 |
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki, amekutana na kufanya Mazungumzo na Rais wa Jamhuri
ya Uganda Mheshimiwa Yoeri Kaguta Museveni, ambapo pamoja na mambo mengine
wamekubaliana kujengwa kwa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Bandari ya Tanga
nchini Tanzania hadi nchini Uganda.
Rais Museveni
amemtembelea Rais Magufuli katika Ikulu ndogo ya Arusha leo jioni mara baada ya
kuwasili hapa nchini akitokea nchini Uganda, ambapo hapo kesho atahudhuria
Mkutano Mkuu wa 17 wa kawaida wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, utakaofanyika katika Hoteli ya Ngurudoto Jijini Arusha.
Akizungumza baada ya
viongozi hao kufanya mazungumzo ya faragha, Rais Magufuli amesema wamekubaliana
kutekeleza mradi huo wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Tanga hadi Uganda,
kwa manufaa ya nchi zote mbili na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Amesema bomba hilo
litakuwa na urefu wa kilometa 1,120 na kwamba mradi huo utazalisha ajira za watu
zaidi ya 15,000.
Rais Magufuli
ameongeza kuwa pamoja na kujengwa kwa bomba la mafuta, pia wamezungumzia
kuongeza biashara ndani ya nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki, kujenga viwanda
na kuzalisha ajira zaidi kupitia sekta mbalimbali za uzalishaji mali.
Aidha, Rais Magufuli
amesema katika Mkutano huu nchi wanachama watajadili maombi ya nchi ya Sudan
Kusini kupata uanachama ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amebainisha kuwa,
kwa Sudan Kusini kuwa mwanachama Jumuiya ya Afrika Mashariki, itakuwa na uwezo
wa kufanya biashara katika eneo lenye takribani watu milioni 150 na hivyo
kupata manufaa makubwa zaidi.
Kwa upande wake Rais
Yoeri Kaguta Museven pamoja na kuunga mkono yaliyosemwa na Rais Magufuli
amempongeza kwa kasi yake nzuri aliyoanza nayo katika uongozi, na amesema ni
matumaini yake kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, sasa
zitakuwa katika nafasi nzuri ya kwenda kwa kasi ya Rais Magufuli katika
maendeleo.
Gerson Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
01 Machi,
2016
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni